Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya kulinda amani Ivory Coast vyaongezwa kwenye maeneo ya ukaguzi

Vikosi vya kulinda amani Ivory Coast vyaongezwa kwenye maeneo ya ukaguzi

Vikosi vya kulinda amani nchini Ivory Coast vimeongezwa katika kile kinachoonekana ni kukabiliana na hali ya wasiwasi katika vituo vya ukaguzi kufuatia tukio la shambulizi lililosababisha vifo vya watu wanne.

Watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari walifyatua risasi kuwalenga askari wa serikali waliokuwa wakiweka doria kwenye vituo vya ukaguzi katika kijiji cha Iribo kilichopo umbali wa kilometa 90 kutoka mji mkuu Abidjan. Tukio hilo limetokea August 25.

Katika majibizano ya risasi, askari mmoja wa serikali, raia mmoja wa kawaida na wavamizi wawili walipoteza maisha. Tukio hilo limekuja katika wakati ambapo Baraza la Usalama likipitisha azimio nambari 2062 linalotaka kupunguzwa kwa idadi ya askari wa kulinda amani kutokana na hali ya mambo kuanza kutengamaa.

Lakini kutokana na hali hiyo ya mambo, vikosi vya kulinda amani vilivyopo nchini humo vimeongezwa katika maeneo ya ukaguzi kujaribu kudhibiti hali yoyote korofi.