Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yaendelea kukagua hali ya mambo Haiti baada ya Tufani ya Isaac

OCHA yaendelea kukagua hali ya mambo Haiti baada ya Tufani ya Isaac

Ofisi ya mratibu mkuu wa misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA, inaendelea kufanya ukaguzi wa uharibifu ulofanyika nchini Haiti kutokana na tufani ijulikanayo kama Isaac hivi karibuni. Watu sita wameripotiwa kufariki dunia kutokana na tufani hiyo, akiwemo msichana mwenye miaka 8.

Maeneo 41 ya makazi ya dharura yamefunguliwa huku vyakula na maji vikisambaziwa watu katika maeneo hayo. Idara ya kitaifa ya tahadhari na majanga inaripoti kuwa zaidi ya watu 14, 000 wameokolewa kutokana na tufani hiyo, huku watu zaidi ya 13, 000 wakiwa wamehamishiwa kwenye makazi ya muda ya dharura.

Kwa mujibu wa Vanessa Huguenin kutoka kwa ofisi ya OCHA, bado mvua nzito inaendelea kunyesha nchini Haiti, na OCHA inaendelea kukagua uharibifu na uwezekano wa kuongezeka visa vya maradhi ya kipindupindu.