Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yatoa wito hatua ichukuliwe kulinda jitihada za amani katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini

UNMISS yatoa wito hatua ichukuliwe kulinda jitihada za amani katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Sudan Kusini, UNMISS, umetoa wito kwa taasisi zote katika Sudan ya Kusini na wadau wengine wanaohusika katika kuimarisha jimbo la Jonglei kuchukuwa hatua mara moja, ili kulinda ufanisi uliofikiwa katika jitihada za kutafuta amani, kukomesha ukiukaji wa haki za binadamu katika kata ya Pibor, na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.

Hali ya usalama katika jimbo la Jonglei imeimarika kwa kiasi kikubwa tangu ghasia za kikabila zilipoyakatili maisha ya mamia ya watu mwanzoni mwa mwaka huu. Juhudi za kupongezwa zimefanyika katika kuongeza usalama na kuwalinda raia na mali zao. Hata hivyo, UNMISS imetiwa wasiwasi na kuongezeka kwa ukiukaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na baadhi ya watu katika jeshi la Sudan Kusini, SPLA katika kata ya Pibor. Vikosi vya SPLA vimepelekwa katika kata hiyo kusaidia mpango wa serikali wa kuondoa silaha mikononi mwa raia, kama sehemu ya mpango mzima wa amani.

Kati ya Julai 15 na agosti 20, timu za waangalizi wa UNMISS ziliripoti ukiukaji wa haki za binadamu, ukiwemo mauaji ya mtu mmoja, shutuma 27 za utesaji, visa 12 vya ubakaji, na 8 vya utekaji nyara. Wengi wa waathirika ni wanawake na katika baadhi ya visa, ni watoto.