Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam huru wa UM wahimiza kukomeshwa ukatili dhidi ya wanaotetea haki za binadamu Bahrain

Wataalam huru wa UM wahimiza kukomeshwa ukatili dhidi ya wanaotetea haki za binadamu Bahrain

Kundi la wataalam huru wa Umoja wa Mataifa, leo limeelezea wasiwasi wake kuhusu kampeni ya ukatili unaotekelezwa na uongozi wa Bahrain dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo. Wataalam hao wameitaka serikali ya Bahrain kumwachilia huru mara moja mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu, Nabeel Rajab, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela hivi karibuni.

Nabeel Rajab alihukumiwa na hatia tatu zilizohusiana na kufanya mikutano ya amani na kufanya maandamano kupinga kukamatwa na kuzuiliwa kwa mwanaharakati mwenzie, Abdulhadi Al Khawaja.

Tangu mwezi Februari, kumekuwa na vurugu nchini Bahrain, baina ya vikosi vya usalama na waandamanaji, mwaka mmoja tangu maandamano katika nchi mbalimbali yalipoanza katika eneo zima la Ghuba ya Mashariki ya Kati.

Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wamesema huu ndio wakati wa Bahrain kushikamana na haki na uhuru wa kufanya mikutano na kujieleza, na kuwaachilia huru wote waliokamatwa wakati wakitimiza haki zao kihalali.