Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kutatua mzozo wa Syria ni lazima ziendelee:Jan Eliasson

Juhudi za kutatua mzozo wa Syria ni lazima ziendelee:Jan Eliasson

Bado kuna fursa ya kupata suluhu ya kisiasa kwa mzozo wa Syria, amesema naibu Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson.

Katika mahojiano na Maha Fayek wa Radio ya Umoja wa Matifa, Bwana Eliasson amekaribisha kuteuliwa kwa Bwana Lakhdar Brahimi hivi karibuni kama mwakilishi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria.

(SAUTI YA JAN ELIASSON)

"Nadhani kwa Umoja wa Mataifa kuruhusu mzozo uendelee hadi kusababisha mateso ya kupindukia na kwamba tusubiri hadi mzozo huo utatuliwe kwa njia ya kijeshi, si jambo la fahari. Hiyo ni kinyume na kile tunachostahili kufanya. Kwa hiyo, jitihada za masuluhu ya amani ni lazima ziendelee, na ni lazima ziendelee pia kwa hali ya Syria.

Naibu Katibu Mkuu huyo mpya pia amesema kuwa muhula wake katika wadhfa huo utaangazia masuala ya kisiasa na maendeleo.

Eliasson, ambaye ni mwanadiplomasia wa Sweden, amewahi kuhudumu katika Umoja wa Mataifa katika nyadhfa nyingi, ikiwemo kama Mwakilishi Maalum kuhusu Darfur.