Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cambodia ni mfano wa kuigwa maeneo ya Asia na Pacific kwa ajili ya maendeleo endelevu:Hayzer

Cambodia ni mfano wa kuigwa maeneo ya Asia na Pacific kwa ajili ya maendeleo endelevu:Hayzer

Mkuu wa Tume ya Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya maeneo ya Asia na Pasifik, Noeleen Heyzer, amesema kuwa taifa la Camboda linatoa mfano mzuri wa ufumbuzi na uongozi, ambao unahitajika kuigwa na mataifa ya Asia na Pasifiki katika hatua zitakazofuata za kumakinika zaidi katika ukuaji na maendeleo ya kiuchumi. Bi Heyzer amesema hayo katika mkutano na Wizara ya Mazingira ya Cambodia.

Amesema kuwa serikali ya Cambodia imejitahidi sana kwa kipindi cha takriban mwongo mmoja, na kuweka barabara ya maendeleo inayowahusisha wote, kwa kufungua nafasi za kazi ambazo zinaweka na kutimiza viwango vya juu vya ajira, na kwa kufungua masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyake. Amesema kwa kufanya hivyo, Cambodia imekabiliana vyema na mdororo wa uchumi na kuwa na ukuaji endelevu hata wakati uchumi katika eneo zima ulikumbwa na hali ya sintofahamu na mfumko wa bei za bidhaa.

Amesema kuwa taifa la Cambodia lipo kwenye mkondo wa kufikia lengo la maendeleo la milenia la kupunguza umaskini wa kupindukia kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015. Ameongeza kuwa limepiga hatua kubwa pia katika kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa aslimia 50, ingawa bado kuna changamoto za mwanya wa kiuchumi kuzidi kupanuka kati ya wale wanaoishi mjini na wale waishio vijijini.