Shirika la WMO laonya kuhusu ukame wa hali ya juu unaoukabili ulimwengu

21 Agosti 2012

Shirika la Kimataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa, WMO, limesema kuwa ulimwengu unashuhudia ukame ambao ni wa hali ya kipekee. Shirika la WMO limesema ukame unayoikumba Marekani na athari zake dhidi ya bei za chakula kwenye soko la kimataifa, unaonyesha uwezo mdogo wa ulimwengu mzima kustahmili hali kama hii.

Shirika hilo limesema kuwa mwaka huu, chombo cha kupima kiwango cha ukame cha Marekani kimehakiki kuwa kufikia tarehe 31, Julai, asilimia 62.9 ya Marekani ilikuwa inashuhudia hali ya ukame tokea viwango vya wastani hadi viwango vya juu.

Mabadiliko ya misimu nchini India yalisababisha kushuka viwango vya mvua kwa asilimia 50 katika zaidi ya wilaya 600 kote nchini.

Ukame huu unaathiri uzalishaji wa chakula, na shirika la WMO linatoa wito kwa mataifa yaweke sera za kukabiliana na ukame. Australia ndilo taifa pekee lililo na sera ya kukabiliana na ukame kisheria, huku mataifa mengine yakiwa na mipango tu.