Ban azungumzia mkakati mpya wa elimu duniani akiwa Timor Leste

16 Agosti 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuna mkakati mpya wenye lengo la kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa elimu kwenye ajenda ya ulimwengu mzima. Akiwahutubia wanafunzi wa chuo kikuu wa Timor-Leste katika mji mkuu, Dili, Ban ametaja elimu kama kitu cha kipaumbele.

(SAUTI YA BAN Ki-MOON)

Mkakati wa “Elimu Kwanza” utatangazwa rasmi mwezi Septemba, wakati wa mkutano wa Baraza Kuu mjini New York. Bwana Ban amesema kuwa ulimwengu una watu wazima milioni 775 wasiojua kusoma na kuandika, watoto milioni 61 ambao hawapo shule za msingi, na chini ya asilimia 40 ya nchi zinatoa nafasi sawa za elimu kwa watoto wa kike na wakiume.

Baadhi ya malengo ya mkakati wa Elimu Kwanza, ni pamoja na kumpeleka kila mtoto shule, kuboresha viwango vya elimu na kuazizi heshima ya haki za binadamu. Bwana Ban ameandamana na Mjumbe maalum wa Elimu wa Umoja wa Mataifa, Gordon Brown na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Irina Bokova, ambaye pia ametoa kauli kuhusu umuhimu wa elimu.

(SAUTI YA IRINA BOKOVA)

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud