Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya serikali na vya upinzani vimetenda uhalifu wa kivita nchini Syria: ripoti ya UM

Vikosi vya serikali na vya upinzani vimetenda uhalifu wa kivita nchini Syria: ripoti ya UM

Vikosi vya serikali nchini Syria na vile vya upinzani vimetenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Tume huru ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu wakati wa mzozo unaoendelea nchini humo.

Ripoti hiyo ambayo iliidhinishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, inasema kuwa uhalifu wa kivita umetekelezwa kwa viwango vya juu zaidi, na kwamba hali imezorota zaidi, tangu ripoti ya awali ya tume hiyo, ambayo ilitolewa mwezi Februari 2012.

Ripoti hiyo inasema kuwa, uhalifu wa kivita, ukiwemo mauaji, mateso na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu za kimataifa, mauaji kinyume na sheria, uvamizi dhidi ya raia na dhuluma za ngono, umetekelezwa kulingana na sera ya kitaifa, na hivyo kuonyesha kuhusika kwa watu wa tabaka la juu zaidi serikalini, pamoja na vikosi vya usalama. Mapigano nchini Syria yamesababisha vifo vya takriban watu 17, 000 tangu machafuko yalipoanza yapata miezi 17 iliyopita.