Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Valerie Amos kuzuru Syria na Lebanon

Valerie Amos kuzuru Syria na Lebanon

Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, anatarajiwa kusafiri kwenda Syria na Lebanon kuanzia tarehe 14 hadi 16 Agosti. Ziara hiyo ya siku tatu inalenga kuuchagiza ulimwengu kuangazia hali ya kibinadamu inayozidi kuzorota nchini Syria, na athari za mgogoro ama kwa walosalia nchini Syria, au walokimbilia nchi zingine, ikiwemo Lebanon.

Hali ya kibinadamu nchini Syria imezorota zaidi katika majuma machache yalopita, kufuatia mapigano kusambaa tokea mji wa Damascus hadi Aleppo na miji mingine. Watu milioni mbili wanakadiriwa kuathiriwa na mgogoro wa Syria, na zaidi ya watu milioni moja wamefanywa wakimbizi wa ndani. Zaidi ya watu 140, 000 wametoroka machafuko na kukimbilia nchi za Lebanon, Jordan, Uturuki na Iraq.