Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yaomba dola milioni 32.5 kufadhili mahitaji yanayongezeka Myanmar

Mashirika ya kibinadamu yaomba dola milioni 32.5 kufadhili mahitaji yanayongezeka Myanmar

Akikamilisha ziara yake ya siku nne Myanmar, Mkurugenzi wa shughuli za Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadam, John Ging ameelezea hofu yake kuhusu hatma ya zaidi ya nusu milioni ya wakimbizi wa ndani, na kutoa wito ziheshimiwe kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu ili kuyawezesha mashirika ya kutoa misaada kuyafikia maeneo yaloathiriwa na mzozo na kuwasaidia walio na mahitaji.

Licha ya juhudi za serikali ya Myanmar katika kuweka amani kote nchini, bado kuna migogoro kwenye jimbo la Kachin, na mizozo ya kijamii kati ya Waislamu na jamii za Rakhine ambazo zimeishi pamoja kwa vizazi vingi imewalazimu watu 64, 000 kuhama makwao kwenye jimbo la Rakhine.

Bwana Ging amesema huu ndio wakati wa mabadiliko Myanmar, akitaja kwamba kwa upande mmoja kuna maendeleo yanayotokana na kuweka demokrasia, amani na maendeleo ya kiuchumi, lakini kwa upande mwingine, migogoro na mizozo ya kijamii inaweza kudhoofisha amani na utulivu, na kulazimu kuwepo mahitaji makubwa ya kibinadamu.