Ban asikitishwa na hali ya usalama DRC

7 Agosti 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hasa kutokana na ghasia zinazochochewa na kundi la M23 na makundi mengine yenye silaha, yakiwemo ya kitaifa na ya kimataifa. Bwana Ban amesema haya katika ujumbe wake kwa kongamano la kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu, mjini Kampala, Uganda, ambalo linaangazia

hali mashariki mwa Kongo.

Amesema athari za kibinadamu kwa raia zimekuwa mbaya sana, na kwama kuendelea kuzorota kwa hali kunatishia usalama na utulivu katika eneo zima la Maziwa Makuu.

Bwana Ban ametaja kuwa ingawa vitendo vya M23 vilipungua mwezi Julai, anatoa wito kwa kundi hilo la waasi likomeshe kabisa uchochezi wa machafuko mara moja.

Amelaani ghasia na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulotekelezwa na M23 na makundi mengine dhidi ya raia, na kuongeza kuwa wahusika wote ni lazima wachukuliwe hatua za kisheria.

Ameelezea pia kusikitishwa kwake na ripoti kuwa kundi la M23 linaungwa mkono kutoka nje ya Kongo, na kutoa wito msaada kama huo ukomeshwe mara moja.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter