Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika ni lazima izingatie Biashara ya Kilimo kwa Uchumi Wake:Yumkella

Afrika ni lazima izingatie Biashara ya Kilimo kwa Uchumi Wake:Yumkella

Bara la Afrika linahitaji kutilia maanani mseto wa uchumi pamoja na bishara ya kilimo ili kuweza kuliinua bara hilo kutoka umaskini na kuliweka kwenye mkondo wa maendeleo. Hii ni kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu kutoka kwenye Umoja wa Mataifa. Mkurugenzi mkuu wa shirika la maendeleo ya kiviwanda la Umoja wa Mataifa Kandeh K. Yumkella amesema kuwa kilimo ni sekta muhimu kwenye uchumi wa bara la Afrika na ndiye mkombozi wake kutoka kwenye umaskini.

Pia uwekezaji kwenye sekta ya usafiri , kawi na maji pamoja na kwenye teknolojia ya mawasiliano na habari ni muhimu kwenye ustawi wa biashara ya kilimo. Yumkella aliyatamka haya kwenye mkutano mjini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mkutano uliowaleta pamoja mawaziri wa fedha , magavana wa benki kuu na washirikishi wa mashirika ya maendelo ya kimataifa pamoja na taasisi za kifedha ambapo alikuwa mzungumzaji mkuu.