Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu Ahimiza Kukomeshwa Umwagaji damu na kuelezea Hofu kuhusu Mapigano Makali Aleppo, Syria

Katibu Mkuu Ahimiza Kukomeshwa Umwagaji damu na kuelezea Hofu kuhusu Mapigano Makali Aleppo, Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito kwa pande zote husika kwenye mzozo wa Syria kukomesha umwagaji damu, na kuelezea hofu yake kuhusu mapigano na matumizi ya silaha nzito nzito kwenye mji wa Aleppo, ambao ndio mji wenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo. Bwana Ban ambaye amerejea kutoka ziara yake Uchina, Kusini Mashariki mwa Ulaya na London, amesema kwenye ziara yake nzima alikuwa anawazia hali mbaya na isokubalika nchini Syria.

Amesema ingawa Mkuu wa Huduma za Kulinda amani katika Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous amekutana hivi karibuni na wawakilishi wa pande zote na kusisitiza kuwa serikali ikomeshe matumizi ya silaha nzito, na pande zote kusitisha ghasia, wito huo haujatiliwa maanani.  

Amesema kila uchao, kadri machafuko yanapozidi kuchacha, raia wengi zaidi wa Syria wanauawa, wanateswa, au kulazimika kuhama makwao na nchi yao. Amesema ghasia zaidi zimefanya Waangalizi wa Umoja wa Mataifa, UNSMIS, kutimiza majukumu yao kuwa mgumu.