Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa Dola milioni 20 Kuwasaidia Wakimbizi Sudan Kusini

UM watoa Dola milioni 20 Kuwasaidia Wakimbizi Sudan Kusini

Mratibu wa huduma za dharura kwenye Umoja wa Mataifa OCHA, Bi. Valerie Amos, leo ametangaza kuwa shirika hilo limetenga zaidi ya dola milioni ishirini kuwasaidia watu wanaokimbilia Sudan Kusini wakitoroka mapigano katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Bi. Amos amesema kuwa takriban watu 170, 000 wamekimbia makwao kwa sababu ya vita na njaa, na bado watu wengine wapo njiani wakielekea Sudan Kusini. Amesema, wakimbizi hao wanapowasili Sudan Kusini wanahangaika na maisha, akiongeza kuwa wengi wanapoteza maisha yao kutokana na maradhi yanayozuilika kutokana na hali ya hatari na idadi kubwa kupindukia ya watu kwenye kambi. Ameiomba jumuiya ya kimataifa kufanya juhudi za pamoja, ili waweze kukabiliana na mgogoro huo.

Hali ya wakimbizi imezorota zaidi hivi karibuni, kutokana na rasilmali kuendelea kuwa adimu. Aidha, mashirika ya kutoa huduma za kibinadam yanapata ugumu kutoa huduma kutokana na idadi ya wakimbizi inayoendelea kuongezeka.