Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu mpya achukua usukani UNSMIS

Mkuu mpya achukua usukani UNSMIS

Mkuu mpya wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, UNSMIS, amesema anatarajia kupungua kwa kiwango cha machafuko wakati wa kipindi cha mwisho cha operesheni ya UNSMIS nchini humo.

Luteni Jenerali Babacar Gaye, ambaye amekaribishwa kwa waandishi wa habari mjini Damascus siku ya Jumatano, amesema anashika usukani wakati mgumu sasa.

Hata hivyo, amesema kuwa UNSMIS inarejea ikiwa na matumaini kuwa, kutakuwa na busara, na kwamba watapata mwanga angaa kidogo kuwa ghasia zitapungua, na kila fursa itatumiwa katika kipindi hiki kifupi kupunguza mateso kwa watu wa Syria.

Jenerali Gaye, ambaye ni raia wa Senegal, anamrithi Jenerali Robert Mood, ambaye alisitisha shughuli za UNSMIS kati mwa mwezi Juni kwa sababu ya ongezeko la machafuko, na ambaye muhula wake wa kazi hiyo ulimalizika Julai 20.