Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama larefusha muda wa kusalia vikosi vya kulinda amani Cyprus

Baraza la Usalama larefusha muda wa kusalia vikosi vya kulinda amani Cyprus

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha muda wa kusalia kwa vikosi vya kulinda amani nchini Cyprus hadi kufikia January 2013 huku pia likiwataka viongozi wa pande mbili Ugiriki ya Cyprus na wale wa Uturuki Cyprus kuongeza juhudi za majadiliano ili kukwamua mkwamo unaoliandama eneo hilo.

Katika azimio lake liliungwa mkono na nchi 13, wanachama hao wametaka pande hizo kukaribia nukta muhimu kwa kushiriki kikamilifu kwenye majadiliano ambayo ndiyo dira ya kutanzua mkwamo wa mambo.

Wakati wa upigaji kura ili kupitisha azimio hilo, nchi za Azerbaijan na Pakistan ziliweka kando kura zao. Vikosi hivyo vya kulinda amani vilipelekwa kwenye eneo hilo tangu mwaka 1964 wakati kulipozuka machafuko kwa mara ya kwanza.

Kwa miaka kadhaa sasa Umoja wa Mataifa umechukua shabaha ya usoni kufanikisha majadiliano ya pande zote mbili ili kuleta kwenye ukomo mgongano huo.