Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aliomba Baraza la Usalama Kutekeleza Wajibu Wake na Kuchukua Hatua ya Pamoja kuhusu Syria

Ban aliomba Baraza la Usalama Kutekeleza Wajibu Wake na Kuchukua Hatua ya Pamoja kuhusu Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutimiza wajibu wake na kuchukuwa hatua ya pamoja kuhusu hali iliyopo nchini Syria, chini ya majukumu ya mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Ban amesema, hakuna muda wa kupoteza, na kwamba watu wa Syria wameteseka kwa muda mrefu sana. Ameongeza kuwa umwagaji damu ni lazima ukomeshwe sasa.

Akielezea kushtushwa kwake na kuongezeka kwa ghasia nchini Syria, Bwana Ban amelaani vikali shambulizi la bomu hapo jana katika makao makuu ya usalama wa kitaifa mjini Damascus, ambayo yaliwaua na kuwajeruhi watu kadhaa, wakiwemo maafisa wa serikali. Amesema vitendo vya ghasia vinavyotekelezwa na upande wowote ule ni ukiukaji wa mpango uliowekwa wa amani, wenye vipengee sita.

Ameelezea pia kusikitishwa kwake na matumizi ya silaha nzito nzito yanayofanywa na vikosi vya usalama vya Syria dhidi ya raia, ikiwemo katika mji wa Damascus, licha ya serikali kutoa hakikisho kuwa silaha kama hizo hazingetumika tena.