Dhuluma za ngono dhidi ya raia Syria zafaa kukomeshwa mara moja: UM

16 Julai 2012

Wakati mzozo wa Syria unazidi kutokota, watu wa Syria wanaendelea kuteseka hata zaidi. Raia ambao tayari wamebaniwa katika mviringo wa ghasia, sasa pia wanalengwa na dhuluma za ngono, amesema kaimu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu dhuluma za ngono katika maeneo ya vita, Vijay Nambiar. Amesema serikali zote zina jukumu la kuwalinda raia kutokana na vitendo kama hivyo vya uhalifu, na kutoa wito kwa serikali ya Syria kutekeleza wajibu wake.

Ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo sasa linajadili mswada wa azimio jipya kuhusu Syria, lisiwasahau waathirika wa ukatili wa ngono nchini humo. Amesema ripoti za hivi karibuni za dhuluma za ngono dhidi ya wanawake, watoto na hata wanaume zinazotekelezwa na wanajeshi wa serikali na makundi yenye silaha ya Shaniha, zinasikitisha.

Kwa mujibu wa ripoti ya tume huru ya kimataifa ya uchunguzi kuhusu Syria, ubakaji, ukiwemo wa magenge dhidi ya mtu mmoja, yalifanywa hasa zaidi wakati wa msako ndani ya nyumba za watu, wakati vikosi vya serikali vilipoingia mijini na vijijini, na wakati wa kuwahoji watu kizuizini.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter