Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifaa vya kujenga amani vyahitaji kuboreshwa, laambiwa Baraza la Usalama la UM

Vifaa vya kujenga amani vyahitaji kuboreshwa, laambiwa Baraza la Usalama la UM

Mwisho wa mzozo kawaida haumaanishi amani imewasili. Hii ndio mojawepo ya sababu za Umoja wa Mataifa kuunda Tume ya Kujenga Amani. Lakini ili ujenzi wa amani utendeke kwa njia inayofaa, ni lazima vifaa vinavyotumiwa katika ujenzi huo viendelezwe na kuimarishwa, vikiwemo kutoa ufadhili wa kifedha ufaao kwa mataifa husika, ili kuendeleza miradi ya kujenga amani.

Tume hiyo ambayo iliundwa mwaka 2005, ina jukumu maalum la kuwaleta pamoja wahusika wote, kuratibu rasilmali, na kutoa mawaidha kuhusu mbinu za kujenga amani na maridhiano baada ya mzozo au vita, na kutambua mapengo yoyote ambayo yanaweza kusababisha kuzorota amani tena.

Haya yamejitokeza katika maelezo ya tume hiyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kikao chake cha tano, katika mjadala ambao uliandaliwa na ubalozi wa Colombia kwenye Umoja wa Mataifa, ambao unashikilia urais wa Baraza hilo kwa mwezi Julai. Akizungumza wakati wa mjadala huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema, kuna kazi nyingi ya kufanya, kwani bado kuna maswali kuhusu kazi na umuhimu wa idara zilizowekwa kwa ajili ya ujenzi wa amani.