Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yazitaka nchi kuunda Sheria zitakazosaidia Masuala ya HIV na Sio Kinyume

UNAIDS yazitaka nchi kuunda Sheria zitakazosaidia Masuala ya HIV na Sio Kinyume

Tume ya kimataifa ya sheria na masuala ya HIV imezindua ripoti yake ya mwaka 2012 mjini New York inayopinga sheria zinazokandamiza haki za binadamu na vita dhidi ya ukimwi na kutoa mapendekezo ya kushughulikia tatizo hilo. Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae ambaye pia ni mjumbe wa tume hiyo amesema hivi sasa kuna ufuatuiliaji mkubwa sana wa jukumu la sheria katika vita dhidi ya ukimwi kuliko wakati mwingine wowote, na kilichobainika ni kwamba kuna tatizo la sheria mbaya ambazo zinagharimu maisha ya watu. Ametaka sheria hizo zikomeshwe na kuundwa sheria ambazo zinafuata ushahidi na kutekeleza haki za binadamu.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS limesema unyanyapaa, ubaguzi na mitazamo mikali ya kisheria kwa mda mrefu imekuwa ikichukuliwa kama kikwazo katika mapambano dhidi ya kimwi hususani kwa makundi ya watu wasiojiweza na wanaohitaji msaada zaidi. Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe amesema umuhimu wa ripoti hiyo ni kwamba imekwenda ndani zaidi ya unyanyapaa na ubaguzi na kuhoji sheria na mitazamo inayokiuka haki za binadamu kwa watu wenye HIV. Ripoti imetoa mapendekezo ambayo yanajumuisha maoni ya serikali na jumuiya za kijamii.