Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malengo ya Maendeleo ya Milenia:baadhi yametimizwa, lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya

Malengo ya Maendeleo ya Milenia:baadhi yametimizwa, lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya

Kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa wanaohusika na masuala ya umaskini, maji na usafi, elimu, afya, chakula, mshikamano wa kimataifa na madeni ya nje, limeonya leo kuwa hakuna wakati wa kupoteza huku kukibaki tuu miaka mitatu kufikia 2015, ambao ni mwaka wa mwisho wa kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Kundi hilo limetoa wito kwa mataifa kuongeza jitihada zao ili kuhakikisha utekelezaji kamili wa lengo kuu la haki za binadamu kwa wote.

Ripoti ya 2012 kuhusu Maendeleo ya Milenia, iliyochapishwa wiki iliyopita, inamulika mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya malengo hayo ya maendeleo. Hata hivyo, wataalam wa Umoja wa Mataifa wamesema kuna masuala kadhaa yanayohitaji kushughulikiwa haraka, na kutoa wito kwa serikali kote duniani kuimarisha juhudi zao ili kufikia Maendeleo ya Milenia na wakati huo huo kuhakikisha kwamba baada ya 2015, ajenda ya maendeleo itakuwa na msingi wa haki za binadamu.

Wameongeza kuwa viwango vya haki za binadamu vinatoa mfumo unaohakikisha kuwa kazi ya kuleta maendeleo itatekelezwa kulingana na maadili ya kimataifa, lakini pia kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa njia ya usawa, haki na ilio endelevu.