Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyama vya Siasa Afrika vyakutana Tanzania Kujadilia Ufadhili wa Fedha

Vyama vya Siasa Afrika vyakutana Tanzania Kujadilia Ufadhili wa Fedha

Makundi ya kisiasa barani afrika yameanza mkutano wa siku tatu nchini Tanzania kwa shabaha ya kujadilia nafasi ya vyama vya kisiasa pamoja na mwelekeo mpya wa ufadhili wa mafungu ya fedha.

Wajumbe kwenye mkutano huo ambao umefunguliwa na makamu wa rais Dr Gharib Bilal wanatazamia kumulika nafasi ya vyama vya siasa nanma vinavyoweza kushiriki kwenye ujenzi wa demokrasia na wakati huo huo kuwavutia wapiga kura katika mazingira ya amani na utulivu.

Kutoka DSM, George Njogopa anatupia macho mkutano huo ambao umewajumuisha wajumbe kutoka mataifa 11, na taasisi kadhaa kutoka barani Ulaya.

Jambo kubwa linalozingatiwa kwenye kongamano hili ambalo linaratibiwa na kituo cha demokrasia ni kuangalia kwa kiasi gani vyama vya siasa vinaweza kupata ufadhili wa fedha kwa ajili ya kuendesha kikamilifu harakati za kisiasa pasipo kujiingiza kwenye mikondo ya ukusanyaji wa fedha haramu.

Sheria iliyopitishwa hivi karibuni na serikali ya Tanzania inayoangazia matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi, ni moja ya kipengele kinachotazamiwa kutumiwa na wajumbe wa mkutano huu.

Kuna wasiwasi kwamba bila kuweka misingi na sheria mujarabu kwa ajili ya kuvimulika vyama vya siasa jinsi vinavyopata mafungu ya fedha, kunaweza kutoa mwanya kwa vyama hivyo kukusanya fedha kutoka vyanzo haramu jambo ambalo linaweza kusababisha mgongamo wa kimaslahi pindi vinapofaulu kukamata dola.

Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba anasema kuwa, kufanyika kwa mikutano ya jinsi hii kunatoa fursa ya kipekee hasa wakati huu ambapo kunashuhudia machipuoa mapya ya kisasa barani Africa.

Mjumbe mmoja kutoka nchini Ghana alisema uzoefu wa mataifa mengi barani afrika unaonyesha kuwa vyama vya kisiasa havipati mafungu ya fedha toka serikalini kama ilivyo kwa Tanzania hivyo mkutano huo unatazamia pia kufungua njia ya kukwamua tatizo hilo.

Akituwama kwenye mada hiyo hiyo Bi Nderkindo Perpetua Kessy ambaye ni mbunge wa bunge la afrika mashariki alisisitiza umuhimu wa kuziipa msukumo wa pekee rasilimali zinazopatikana barani afrika kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kufungua majadiliano mazuri ya namna ya kuvifadhilia vyama vya kisiasa.

Katika hotuba yake, Makamu wa rais Dr Gharib Bilal alizingatia maeneo kadhaa ikiwemo lile la kuvitaka vyama vya kisasa kutekeleza majukumu yake kwa kufuata miiko inayotambulika bila kujiingiza katika mienendo ya hila na gilba gilba.

Mkutano huo unatazamia kufikia kikomo chake hapo siku ya alhamisi ambako wajumbe watayatangaza maazio yaliyofikiwa.