Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria Mbaya na Ukiukaji wa Haki za Binadamu ni Kikwazo katika Vita dhidi ya Ukimwi:UM

Sheria Mbaya na Ukiukaji wa Haki za Binadamu ni Kikwazo katika Vita dhidi ya Ukimwi:UM

Sheria za kuadhibu watu pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu unaongeza vifo kutokana na Ukimwi, uharibifu wa fedha na kuwa kizuizi katika vita vya kimataifa dhidi ya Ukimwi, imesema ripoti ya tume huru ya kimataifa kuhusu Ukimwi na sheria, ambayo inawahusisha viongozi na wataalam.

Tume hiyo iliyofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, (UNDP) na Mpango wa Pamoja kuhusu HIV na Ukimwi wa Umoja wa Mataifa, imetoa wito wa dharura kuwekwe sheria zinazolinda haki za binadam ili kuokoa maisha, kupunguza matumizi ya fedha na kuutokomeza Ukimwi. Ripoti hiyo yenye kichwa: Ukimwi na Sheria: hatari, haki na afya, inatoa ushahidi kuwa serikali katika kila eneo la ulimwengu zimepoteza fursa ya mifumo ya kisheria katika kupiga vita Ukimwi.

Ripoti hiyo imetokana na uchunguzi wa kimataifa, uliohusisha ushahidi wa watu zaidi ya 1,000 kutoka nchi 140. Katika zaidi ya nchi 60, ni hatia kumwambukiza mtu, au kumweka katika hatari ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, na zaidi ya watu 600 walio na virusi vya Ukimwi, wamefungwa kwa hatia hiyo katika nchi 24, ikiwemo Marekani.