Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yaweka Tarehe ya Kusikiliza Kesi za Kenya

ICC yaweka Tarehe ya Kusikiliza Kesi za Kenya

Kitengo nambari 5 cha Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa, leo Julai 9 kimeweka tarehe za kuanza kusikilizwa kesi dhidi ya washukiwa wanne wa machafuko yalotokana na uchaguzi uliopita nchini Kenya kama tarehe 10 na 11 Aprili mwaka 2013. Kuwekwa tarehe ya kesi dhidi ya William Samoei Ruto, Joshua Arap Sang, Francis Muthaura na Uhuru Kenyatta, pia kunaweka ratiba ya mambo muhimu ambayo yanatakiwa kufanywa kabla ya kesi hizo kuanza kusikilizwa, ili kuhakikisha haki inatendeka.

Mnamo tarehe 31 Machi 2010, kitengo cha Mahakama hiyo nambari mbili kilimpa mwendeshaji mashtaka idhini ya kufungua uchunguzi kuhusu ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi nchini Kenya na kusababisha vifo vya takriban watu 1, 5000. Kenya ni nchi mwanachama wa ICC tangu mwaka 2005.

Kutokana na uchunguzi huo, washukiwa sita walifika kwa hiari yao wenyewe mbele ya kitengo hicho cha mahakama ya ICC Aprili 7 na 8 2011, na kusikilizwa kwa kesi ya kuhakiki mashtaka dhidi yao kufanyika kati ya Septemba 1 na 9, na Septemba 21 hadi Oktoba 5, 2011. Wawili wao- Henry Kosgei na Muhammed Hussein Ali- waliondolewa mashtaka. Lakini mahakama ilihakiki mashtaka dhidi ya hawa wanne walosalia, na rais wa ICC kuunda kitengo nambari 5 cha mahakama hiyo mnamo tarehe 29 Machi 2012, na kuwasilisha kesi hizi mbele yake.