Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utabiri wa wataalam wa fedha unaathiri bei ya bidhaa za chakula: FAO

Utabiri wa wataalam wa fedha unaathiri bei ya bidhaa za chakula: FAO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula Dunia, FAO, Jose Graziano da Silva, amesema ulimwengu unafaa kuzingatia jinsi utabiri unaofanywa na wataalam kwenye masoko ya fedha na hisa unavyoathiri bei za chakula.

Bwa da Silva amesema hayo kwenye mjadala wa ngazi ya juu kuhusu swala la mfumko wa bei ya chakula kwenye makao makuu ya FAO mjini Rome.

Bwana da Silva amesema, ingawa kumefanywa uchunguzi na ukaguzi mkubwa kuhusu mfumko wa bei ya bidhaa za chakula, ufahamu zaidi unahitajika kuhusu athari za utabiri unaofanywa kwenye masoko ya fedha.

Amesema mfumko mkubwa wa bei ya chakula, hasa kwa kasi ambayo umekuwa ukifanyika tangu mwaka 2007, unaathiri vibaya zaidi maisha ya watu maskini, na pia wakulima maskini kote duniani.