Baraza la Haki za Binadam lalaani ukiukaji wa haki nchini Mali, Eritrea Ivory Coast na Somalia

6 Julai 2012

Wakati huo huo, Baraza hilo la Haki za Binadam pia limelaani ukiukaji wa haki za binadam unaotendeka kaskazini mwa Mali, na ambao unaenezwa na waasi, makundi ya kigaidi na mitandao mingine ya kihalifu kutoka nchi mbalimbali. Limelaani hasa ukatili unaoetendewa wanawake, mauaji, utekaji nyara, uporaji na uharibifu wa maeneo ya urithi wa kiasili na ibada, pamoja na kuajiri watoto katika mapigano, na kuwataka wahusika kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Limeunga mkono juhudi za sasa za Muungano wa nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na Muungano wa Afrika za kutafuta suluhu kwa mzozo wa Mali, na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadam kufuatilia hali ya haki za binadam kaskazini mwa Mali na kutoa ripoti kwenye kikao cha 21 cha Baraza hilo.

Baraza hilo pia limelaani vikali ukiukaji wa haki za binadam nchini Eritrea, ukiwemo kubana uhuru wa vyombo vya habari na kuwalazimu wananchi kuingia katika jeshi, na kumteua mtaalam maalum kuhusu hali ya haki za binadam nchini humo. Aidha, limeongeza mihula ya wataalam huru kuhusu haki za binadam nchini Ivory Coast na nchini Somalia, na kulaani ukiukaji wa haki za binadam kwa mashambulizi dhidi ya raia katika nchi hizo mbili, na mauaji ya walinda amani 7 wa Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud