Hali nchini Mali inatishia amani ya kimataifa: Baraza la Usalama

5 Julai 2012
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limesema hali nchini Mali inatishia amani ya kimataifa na usalama katika kanda nzima, na kuazimia kuunga mkono juhudi za  muungano wa kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, katika kushirikiana na serikali ya mpito nchini Mali ili kurejesha uongozi wa kikatiba. 

Katika azimio lake namba 2056 (2012), Baraza hilo limetoa wito kwa wadau wote nchini Mali kuweka mazingira yatakayoiwezesha serikali ya mpito kutekeleza majukumu yake muhimu, na kuhakikisha kurejesha na kulinda mfumo wa uongozi wa kikatiba. Baraza hilo pia limekataa kulitambua kundi linalojiita baraza la kitaifa la kurejesha demokrasia na utaifa (CNRDRE) kama kundi halali, na kulitaka kundi hilo kuvunjwa na wanachama wake kuacha kuingilia masuala ya kisiasa na kazi ya serikali ya mpito.

Baraza la Usalama pia limetoa wito kwa wanajeshi wa Mali kuheshimu utaratibu wa kikatiba, uongozi wa kiraia na haki za binadam, na kulaani vikali kupigwa kwa rais wa mpito, Dioncounda Traoré, mnamo May 21,  mwaka 2012, na kutaka rais huyo aruhusiwe kurejea salama mjini Bamako haraka iwezekanavyo.

Baraza hilo pia limeyataka makundi yote ya waasi kusitisha mapigano yote bila masharti, na makundi yote kaskazini mwa Mali kuacha kukiuka haki za binadam, na kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadam.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter