Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kuondoa sheria za uchongezi Caribean:UNESCO

Ni muhimu kuondoa sheria za uchongezi Caribean:UNESCO

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mjini Kingston, Jamaica, Kwame Boafo, ameelezea kusikitishwa kwake na kuendelea kuwepo sheria za uchongezi kwenye katiba za nchi za eneo la Caribbean, na kuzitaka nchi hizo kuziondoa sheria kama hizo ambazo zinabana uhuru wa vyombo vya habari.

Bwana Boafo amesema hayo kwenye kongamano liloandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Uandishi Habari, (IPI), mjini Port of Spain, Trinidad na Tobago. Kwa mujibu wa jopo la wataalam wengine, sheria ya kuwapata watu na hatia ya uchongezi imetokana na sheria za kikoloni za kubana uhuru wa kujieleza na wa uandishi habari.

Bwana Baoafo kutoka UNESCO amesema kuwa, kuwepo sheria hizo kunakwenda kinyume na kuainishwa mataifa ya eneo la Caribbean kama yenye kuwa na uhuru wa vyombo vya habari, na kwamba ili kuweza kuziondoa sheria kama hizo, ushirikiano na mashirika ya umma yanayopigania uhuru wa vyombo vya habari na taasisi kama IPI utahitajika.

Shirika la UNESCO linapendekeza kuwa sheria za uhusiano wa umma zinatosha kulinda sifa za watu na hakuna haja ya kulinda sifa za watu kutumia sheria zinazokabiliana na uhalifu.