Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani vikali mashambulizi ya kigaidi kwenye makanisa Kenya

Ban alaani vikali mashambulizi ya kigaidi kwenye makanisa Kenya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa siku ya Jumapili dhidi ya makanisa mawili kwenye mji wa Garissa nchini Kenya, na ambayo yalisababisha vifo vya watu 17 na kuwajeruhi wengine wengi.

 Bwana Ban amesema, mashambulizi hayo ambayo yalilenga maeneo ya ibada kwa kukusudia, ni kihalifu na yanafaa kukemewa vikali. Ameongeza kuwa hakuna sababu yoyote inayoweza kukubaliwa kwa kuwalenga raia wasio na hatia bila kubagua.

 Amesema waliotekeleza mashambulizi hayo, na vitendo vingine vya kigaidi nchini Kenya, ni lazima wakabiliwe na mkono wa sheria. Ametuma ujumbe wa rambirambi kwa jamaa wa wahanga wa mashambulizi hayo, na serikali ya Kenya. Akizuru eneo la mashambulizi hayo mapema Jumatatu, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alikuwa na haya ya kusema.

 “Haiwezekani kwa serikali kuweka afisa wa polisi kumlinda kila mtu nchini mwetu. Hivyo, tunataka watu wetu kujua kwamba adui yupo, na tunahitaji kubadilishana habari kote nchini, na kwamba si tu hapa pekee penye hatari.”