Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi 4 wa ICC waachiliwa huru nchini Libya

Wafanyakazi 4 wa ICC waachiliwa huru nchini Libya

Viongozi wa Libya wamewaachilia huru wafanyakazi wanne wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ambao walikuwa wamezuiliwa Zintan, baada ya kumzuru Saif Al-Islam Gaddafi, Juni 7.

Rais wa mahakama ya ICC, Jaji Sang-Hyun Song, ambaye alisafiri kwenda Zintan, amekaribisha uamuzi wa Libya kuwaachilia huru wafanyakazi hao. Bwana Song aliwashukuru viongozi wa Libya na mamlaka za Zintan kwa ushirikiano wao, na kuelezea kuridhishwa kwake kuwa maafisa hao wa ICC walitunzwa vyema wakati wa kuzuiliwa kwao.

Maafisa hao wanne wa ICC, Alexander Khodakov, Esteban Peralta Losilla, Melinda Taylor na Helene Assaf, walikamatwa walipomzuru Said Al-Islam Zintan, katika ziara iliyoidhinishwa na ICC ili kuhakikisha haki za mshukiwa, Al-Islam zinatunzwa wakati akisubiri kesi dhidi yake iliyoko mbele ya mahakama ya ICC.

Serikali ya Libya ilianza kufanya uchunguzi katika ziara hiyo ya maafisa wa ICC. Maelezo ya uchucnguzi huo yaliwasilishwa mbele ya mahakama ya ICC mnamo Juni 22, na Bwana Song amesema uchunguzi zaidi utafanywa kuhusu maelezo hayo watakapowasili mjini The Hague maafisa hao walioachiliwa huru.