Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wito watolewa kuumaliza mzozo wa Syria na kuweka serikali ya mpito

Wito watolewa kuumaliza mzozo wa Syria na kuweka serikali ya mpito

Kundi la kuchukua hatua la Umoja wa Mataifa, limefikia makubaliano kuhusu hatua zinazohitajika kuchukuliwa haraka, ili kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini Syria. Akisoma taarifa ya matokeo ya mkutano wa kundi hilo mjini Geneva Jumamosi, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu, Kofi Annan, amesema hakuna muda wa kupoteza, na kwamba ingawa ni wajibu wa watu wa Syria kupata suluhu kwa mzozo huo, mazingira ni lazima yawepo ya kuwezesha kufanya hivyo haraka. Limewataka wahusika katika mgogoro huo kuzingatia tena na kutekeleza mpango wa kimataifa wa amani wenye vipengee sita, na kusitisha aina zote za ghasia.

Kundi hilo limezitaka pande zote ziafikie serikali ya mpito itakayowajumuisha watu kutoka serikalini na katika upinzani, na isiyopendelea upande wowote.

Serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kuifanyia mabadiliko katiba, na kusimamia uchaguzi huru na wa haki, ili kuwezesha mabadiliko ya kisiasa ya kidemokrasia, yatakayokwenda sambamba na matakwa ya watu wa Syria. Bwana Anan amesema mazungumzo zaidi yatafaywa ili kuweka ratiba ya shughula za serikali ya mpito.

 “Ni wajibu wa watu wa Syria kupata muafaka wa kisiasa, lakini hatuna muda wa kupoteza. Tunahitaji hatua za haraka kufikia muafaka. Mgogoro huu ni lazima utatuliwe kupitia mazungumzo ya amani pekee. Mazingira yanayowezesha suluhu ya kisiasa ni lazima yawepo. Umwagaji damu ni lazima ukomeshwe. Jamii ya kimataifa i tayari kutoa msaada muhimu katika kutekeleza yale yatakayoafikiwa na wahusika katika mzozo huu. Kundi la kuchukuwa hatua litaingilia inavyopaswa, ili kutoa shinikizo la pamoja kwa wahusika Syria, kutekeleza yale tumekubaliana, na linapinga hatua zozote zaidi za kijeshi katika mzozo huu.”

Mkutano wa kundi hilo la kuchukuwa hatua uliwajumuisha wawakilishi wa mataifa wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, Iraq, Kuwait na Qatar. Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Nabil ElAraby.