Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima njaa itokomezwe, Ban aiambia Kamati kuhusu Usalama wa Chakula

Ni lazima njaa itokomezwe, Ban aiambia Kamati kuhusu Usalama wa Chakula

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesimamia kikao cha kamati maalum kuhusu usalama wa chakula duniani.  Ban amekaribisha matokeo thabiti ya mkutano wa Rio+20 kuhusu usalama wa chakula na lishe. Kufuatia kuzinduliwa kwa mchakato wa kutokomeza njaa wiki ilopita, kamati hiyo maalum itaelekezwa tena kuzingatia malengo matano muhimu ya mchakato huo, kama mwongozo wa mfumo thabiti wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha usalama wa chakula na lishe.

Pia amesema, tangu ianzishwe kamati hiyo maalum mwaka 2008, imepiga hatua katika kuweka mchakato wa kina wa kuchukua hatua kwa ajili ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wa usalama wa chakula, hasa katika matukio ya hivi karibuni ya uhaba wa chakula. Amesema, mchakato huo ulisaidia katika kuchagiza mitazamo ya ushirikiano miongoni mwa mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Rio, na katika mikutano ya G8 na G20.

Bwana Ban amesema, takriban watu bilioni 1 bado wanapitia njaa kila wakati, na kutoa wito kwa mashirika, serikali, wafanyabiashara, mashirika ya umma na wanasayansi kutokomeza njaa kabisa.