Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fursa ya watu kukusanyika kwa amani inazidi kutoweka-Kiai

Fursa ya watu kukusanyika kwa amani inazidi kutoweka-Kiai

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa, kuhusu haki ya kufanya mikutano ya amani, Maina Kiai, ametoa wito kwa serikali zote na jamii ya kimataifa kuchagiza na kulinda haki ya kuwa na uhuru wa kufanya mikutano ya amani na watu kushirikiana, ambayo hukiukwa au imo hatarini katika baadhi ya mataifa.

Amesema, inashangaza jinsi serikali zinavyokiuka haki za watu kufanya mikutano ya amani, kukiuka haki yao ya kuishi na kulindwa kutokan na dhuluma, ilhali haki hizi hazina kikomo.

Bwana Kiai amesema haya wakati akiwasilisha ripoti yake ya kila mwaka kwa Baraza la Haki za Binadamu, na ambayo ina mapendekezo kadhaa ya kuweka kiwango cha wastani cha kulinda haki ya kuwa na uhuru wa kufanya mikutano na kuwa na uhusiano na watu wengine. Ametaka uhuru wa kufanya mikutano uwe haki, na vizuizi vondolewe. Ameongeza kuwa haki hii imepuuzwa kwa muda mrefu katika sheria za kimataifa zinazohusu haki za binadamu.