Muafaka wafikiwa kuhusu mswada wa mkataba wa Rio+20

19 Juni 2012

Wawakilishi wa serikali na wadau kutoka kote ulimwenguni wamefikia muafaka kuhusu mswada wa mkataba wa maendeleo endelevu wa Rio+20, ambao unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mkutano wa viongozi mjini Rio de Janeiro, Brazil, ambao, ambao unaanza rasmi hapo kesho.

Katika mswada huo, viongozi wa kimataifa wanaazimia kuunga mkono maendeleo endelevu na kuhakikisha kuwa maendeleo yote ya kiuchumi na kijamii yanajali mazingira kwa njia endelevu kwa ajili kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Kutokomeza umaskini kumepewa kipaumbele katika mswada huo, kama changamoto kubwa zaidi inayoukabili ulimwengu. Viongozi hao wanaazimia kuwaokoa wanadamu kutokana na umaskini na njaa, kama suala la dharura.

Wanaazimia pia haja ya kufikia maendeleo endelevu kwa kuunga mkono uchumi unaowahusisha wote, kuweka nafasi zaidi na sawa kwa wote, na kupandisha viwango wastani vya hali ya maisha ta wote, kuunga mkono maendeleo ya kijamii, uhifadhi na matumizi ya rasilmali na mazingira kwa njia endelevu.

Wanaazimia pia kufanya kila juhudi ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015, na kupigania ulimwengu wenye haki, usawa na uhusishaji wa wote katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na uhifadhi wa mazingira kwa njia endelevu, na kutambua kuwa demokrasia, uongozi mzuri na wa kisheria ni muhimu katika kufikia maendeleo endelevu.

Akizungumza baada ya muafaka huo kutangazwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kimoon, ameelezea furaha yake kwa matokeo ya mazungumzo ya awali, na kusema kuwa mswada huo una mambo mengi ambayo yakitekelezwa, yataleta mabadiliko makubwa kote duniani.