Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya FAO, IFAD na WFP yatoa wito kwa mataifa ya G20 kuongeza juhudi za kukabiliana na njaa

Mashirika ya FAO, IFAD na WFP yatoa wito kwa mataifa ya G20 kuongeza juhudi za kukabiliana na njaa

Mashirika ya chakula ya Umoja wa Mataifa, yametoa wito kwa mataifa wanachama wa G20 kwenye mkutano Mexico kuongeza juhudi zao katika kukabiliana na njaa. Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yenye makao mjini Rome, ni FAO, IFAD na WFP.

Yote, kwa taarifa ya pamoja mnamo siku ya Jumanne, yamekaribisha G20 kwa kuendelea kutambua mchango wa wakulima wadogo wadogo katika kuhakikisha usalama wa chakula kote ulimwenguni, na katika kuoneza uzalishaji kwa njia endelevu.

Yamehimiza suala la usalama wa chakula na lishe liendelee kupewa kipaumbele kwenye ajenda ya G20 ya miaka ijayo. Mashirika hayo yameongeza kuwa usalama wa chakula na lishe ni nguzo muhimu katika kuweka amani na utulivu kwa njia endelevu katika siku zijazo, na hivyo ni lazima hili liwe kwenye kila ajenda ya maendeleo endelevu.