Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhuluma dhidi ya wazee ni kukiuka haki za binadamu:Ban

Dhuluma dhidi ya wazee ni kukiuka haki za binadamu:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa dhuluma dhidi ya wazee ni ukiukwaji wa utu na haki za binadamu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO, zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 4 na sita ya wazee kote duniani wamekumbana na dhuluma ya aina moja au nyingine, kimwili, kihisia au kifedha.

Uchunguzi pia unaonyesha kusambaa kwa dhuluma, kupuuzwa na hata vitendo vya ukatili dhidi yao nyumbani na kwenye taasisi wanakokaa wazee.

Kinachosikitisha hata zaidi, amesema Bwana Ban, ni kwamba visa hivi haviripotiwi au kushughulikiwa. Kwa sababu hii, Umoja wa Mataifa umetangaza Juni 15 kama siku ya kimataifa ya kuongeza ufahamu kuhusu dhuluma dhidi ya wazee.

Bwana Ban ametoa wito kwa serikali kote duniani kuweka mikakati ya kina na sheria mwafaka za kuzuia dhuluma kama hizi.