Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Benedict na FAO wajadili Pembe ya Afrika

Papa Benedict na FAO wajadili Pembe ya Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula, FAO, José Graziano da Silva, amefanya mazungumzo na Papa Benedict XVI leo katika mkutano wa faragha, Vatican.

Wakati wa mkutano huo, Bwana da Silva amemwambia Papa Benedict kuwa, kutokomeza njaa ni muhimu, siyo tu kisiasa, kiuchumi na kijamii, bali pia ni wajibu wa kimaadili.

Ametoa wito kwa kanisa kuongeza juhudi zake katika kupiga vita njaa, kwenye daraja ya kimataifa na nyumbani, na pia kuchagiza mtandao wake kote ulimwenguni kuunga mkono lengo la kuwepo usalama wa chakula kote duniani.

Wakati wa Mkutano huo, Papa Benedict alitaka kujua hali ilivyo kwenye pembe ya Afrika, pamoja na mtazamo wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu wa Rio+20.

Kuhusu hilo, Bwana da Silva amesema kuwa usalama wa chakula ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu, na kwamba ni vigumu kuzungumzia maendeleo endelevu ikiwa takriban watu milioni 900 wana njaa.