Vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua vimepungua:UNICEF

13 Juni 2012

Tangu mwaka wa 1990, vifo vya akina mama katika uzazi vimepungua, kwa takriban nusu, na vile vya watoto kushuka kutoka milioni 12 hadi milioni 7.6 mwaka 2010, kwa mujibu wa ripoti mpya, kufuatia uchunguzi chini ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, na mpango wa kuhesabu hatua hadi malengo ya Milenia, hadi 2015.

Baadhi ya mataifa maskini zaidi duniani yamepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto.

Viwango vya vifo vya watoto katika mataifa mengi vimekuwa vikishuka, na vilipungua kwa zaidi ya asilimia 5 wastani kati ya 2000 na 2010, katika mataifa kama Botswana, Misri, Liberia, Madagascar, Malawi, Rwanda na Tanzania.

Mataifa machache kama vile Equatorial Guinea, Nepal na Vietnam, yamepunguza vifo vya akina mama katika uzazi kwa asilimia 75.

Hata hivyo, kila dakika mbili zipitazo, kuna mahali duniani ambako mwanamke anafariki dunia kutokana na matatizo yanayohusiana na uzazi, na uwezekano wa mwanae mchanga kuishi, haupo.

Katika muda huo huo, watoto, 30 hufariki kutokana na magonjwa yanayoweza kuepukika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mataifa ya Afrika na Asia, hayajapiga hatua sana.