Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada zaidi wahitajika Kaskazini mwa Iraq kwa wakimbizi wa Syria

Msaada zaidi wahitajika Kaskazini mwa Iraq kwa wakimbizi wa Syria

Serikali ya jimbo la Kikurdi kaskazini mwa Iraq imetoa wito kwa Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM na mashirika mengine ya kimataifa yatoe msaada zaidi ili kukabiliana na idadi inayoongezeka ya wakimbizi kutoka Syria.

Kwa mujibu wa afisa wa uhamiaji na maendeleo wa serikali ya jimbo hilo, idadi ya wakimbizi wa Syria walioko kwenye kambi ya wakimbizi ya Domiz karibu na mji wa Dahuk, imeonegezeka hadi 3, 500 katika mwezi uliopita.

Takwimu zilizopo hivi sasa zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya wakimbizi 5, 300 wa Syria kaskazini mwa Iraq. Mwishoni mwa mwezi Mei, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilikuwa limesajili wakimbizi zaidi ya 4, 400. Wakimbizi ambao hawaishi kambini wanakaa na jamaa zao au katika miskiti. Wakimbizi wote wanasema kuzorota kwa hali ya usalama na uchumi ndiyo sababu ya wao kutoroka Syria. Jumbe Omar Jumbe amezungumza na UN Radio kutoka Geneva kuhusu hali hiyo.