Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pakistan yakabiliwa na changamoto kubwa:Pillay

Pakistan yakabiliwa na changamoto kubwa:Pillay

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya haki wanawake nchini Pakistan, pamoja na hofu kuhusu mifumo ya sheria nchini humo, ambayo inaonyesha kuhitilafiana.

Bi Pillay amesema haya wakati akihitimisha ziara yake ya siku nne nchini humo, ambako amefanya mikutano na Waziri Mkuu, Yousou Raza Gilani na pia wadau katika maswala ya haki na sheria.

Bi Pillay amesema kuwa Pakistan ipo kwenye nafasi muhimu katika juhudi zake za kuimarisha demokrasia ya umma, na kwamba serikali imepiga hatua fulani muhimu katika maswala ya haki za binadamu. Ameiomba serikali ichukuwe sheria za kimataifa ilizotia saini na kuzijumuisha kwenye katiba na sheria zake.

Ameongeza kuwa ingawa idadi ya wanawake katika nafasi muhimu imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, haki za wanawake hasa vijijini bado zinakiukwa, akitoa mfano wa habari wiki hii kuwa wanawake watano katika kijiji kimoja wamehukumiwa kifo kwa kucheza densi kwenye sherehe ya arusi.