Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yakamilisha kusafirisha raia wa Sudan Kusini

IOM yakamilisha kusafirisha raia wa Sudan Kusini

Shughuli ya siku 24 ya kuwasafirisha karibu watu 12, 000 raia wa Sudan Kusini, imehitimshwa leo na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM.

Safari 79 za ndege zimefanywa ili kuwachukuwa raia hao wa Sudan kusini, ambao walikuwa wamekaa kwenye stesheni ya Kosti kwa miezi kadhaa wakisubiri usafiri kwenda Juba.

Stesheni hiyo ya Kosti ipo takriban kilomita 300 kusini mwa mji Mkuu Khartoum. Wengi wao waliamuwa wenyewe kuruka kwa ndege kwenye shughuli iliyosimamiwa na IOM, baada ya Gavana wa jimbo la White Nile kuwaamrisha waondoke ifikapo tarehe 5 Mei.

Ndege ya mwisho iliondoka saa saba mchana, kwenye operesheni hiyo ya usafirishaji iliyowachukuwa karibu watu 550 kila siku, na ambayo imegharimu dola milioni 5.5 za kimarekani.

IOM sasa inaandaa kuwasafirisha tena raia hao wa Sudan Kusini kuwapeleka kwenye majimbo walikotoka.