Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idara ya Wanawake ya UM Yajiunga kwenye UNAIDS Kupambana na UKIMWI

Idara ya Wanawake ya UM Yajiunga kwenye UNAIDS Kupambana na UKIMWI

Kujumuishwa kwa UN Women kama mshiriki rasmi, ambako kumeidhinishwa leo kwenye mkutano wa halmashauri ya UNAIDS, kunatarajiwa kuimarisha juhudi za shirika hilo zinazohusiana na maswala ya usawa wa jinsia katika kukabiliana na UKIMWI. Pia kunatarajiwa kuongeza ushirikiano na serikali, washirika wa kimataifa, makundi ya wanawake na wanaharakati wa haki za wanawake.

Wakati wa hafla ya idhinisho hilo, Mkurugenzi Mkuu wa UN Women, Michelle Bachelet amesema, anaamini kuwa njia muhimu zaidi ya kukabiliana na virusi vya UKIMWI ni kuwapa wanawake nguvu na kuhakikisha haki zao, ili waweze kujilinda kutokana na maambukizi, wazuie unyanyapaa, na kuweza kupata matibabu.

Usawa wa jinsia na kuheshimu haki za wanawake za uzazi na afya, hasa wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI, ni muhimu katika mpango wa kina wa kukabiliana na UKIMWI.

Idara ya Usawa wa Kijinsia na Kuwapa Uwezo Wanawake (UN WOMEN), imejiunga kwenye juhudi za Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na virusi vya UKIMWI (UNAIDS) kwa ajili ya kufadhili juhudi zake za kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma zinazohusiana na virusi vya HIV.