Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kupiga kura Baraza la Haki za Binadamu lataka uchunguzi Syria

Baada ya kupiga kura Baraza la Haki za Binadamu lataka uchunguzi Syria

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limelaani vikali mauaji ya watu zaidi ya 100 katika kijiji cha Houla, katikati mwa Syria na kuagiza uchunguzi huru ufanyike.

Baraza hilo lililokutana mjini Geneva Ijumaa limepitisha azimio kwa njia ya kura huku wajumbe 41 wakiunga mkono, na watatu wakiwemo Urusi, Uchina na Cuba wakipinga, na wawili kutopiga kura kabisa.

Azimio hili limefikiwa baada ya mswada uliowasilishwa na wajumbe kutoka makundi ya maeneo yote duniani.

Azimio hilo lenye kichwa: Hali Inayozorota ya Haki za Binadamu Nchini Syria na Mauaji ya Hivi Karibuni ya Houleh, linasema jamii ya kimataifa ni lazima ichukuwe hatua kuhusu mauaji ya kinyama na kuteseka kwa watu wa Syria, pamoja na ukatili wa aina yoyote ile unaofanywa na pande zinazohusika katika mzozo wa Syria.

Azimio hilo limerejelea umuhimu wa kutekeleza mpango wa hatua sita wa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na nchi za Kiarabu, Kofi Annan, na kutaja kuwa, hali inaendelea kuzorota kila siku, licha ya wito wa jamii ya kimataifa na jumuiya ya mataifa ya Kiarabu.

Wajumbe waliopinga wanasema azimio hilo linaegemea upande mmoja likishutumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kufumbia macho makundi yenye silaha yanayotishia amani raia wa Syria. Pia wanadai kuwa azimio hilo linachagiza kuingilia uhuru wa taifa huru la Syria.

Kamishina mkuu wa Haki za Binadamu amesema mauji ya Syria yanaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu na ukiukaji wa sharia zingine za kimataifa. Kikao hicho maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu kimeitishwa ili kutathimini kuzorota kwa hali nchini Syria na hasa kutokana na mauaji ya karibuni