Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahitaji ya Kibinadamu Yaongezeka kwenye ghasia za Kivu ya Kaskazini, DRC

Mahitaji ya Kibinadamu Yaongezeka kwenye ghasia za Kivu ya Kaskazini, DRC

Watu 100,000 wamelazimika kutoroka makwao kufuatia ghasia za hivi karibuni katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, mashariki mwa Congo na kupelekea Umoja wa Mataifa kutoa wito zifanywe juhudi bora zaidi za kulinda raia na msaada zaidi kwa walioathirika.

Tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili, maelfu ya jamii katika Kivu ya Kaskazini wamekimbilia usalama wao kufuatia ghasia zilizotokana na wanajeshi kuasi jeshi la kitaifa, pamoja na operesheni za kisiasa za kijeshi za kudhibiti makundi yenye silaha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limesema wiki hii kuwa takriban watu 21, 000 wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani za Rwanda na Uganda. Wakimbizi hawa wanakabiliwa na mahitaji mengi muhimu: jinsi ya kuwalisha watoto wao,  kupata maji safi na jinsi ya kuepukana na maradhi ya kuambukiza kama vile kipindupindu na surua.

Tangu kuzuka mapigano Kivu Kaskazini, msaada mwingi wa kibinadamu umepelekwa kwa wakimbizi wanaofikiwa kwa urahisi kwenye kambi zilizopo karibu na Goma, na wale wanaoishi Rwanda na Uganda. Lakini maelfu ya wengine wamekimbilia maeneo ambayo hayawezi kufikika kwa urahisi, kama vile kwenye misitu, na hawajapata msaada wowote.