Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maafisa wa UM walaani mauaji ya kikatili dhidi ya raia karibu na Homs Syria

Maafisa wa UM walaani mauaji ya kikatili dhidi ya raia karibu na Homs Syria

Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mauaji ya Jumamosi dhidi ya raia zaidi ya 90 wakiwemo watoto 32 na kujeruhi wengine kwa mamia katika kijiji kimoja karibu na mji wa Homs. Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kwamba wahusika wa unyama huo lazima wawajibishwe.

Waangalizi wa mpango wa Umoja wa Mataifa Syria UNSMIS wamethibitisha mauaji hayo baada ya kuangalia maiti kwenye kijiji cha Houla ambako wamethibitisha baada ya uchunguzi kwamba makombora na vifaru vilishambulia makazi ya raia hao.

Taarifa iliyotolewa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na mwakilishi wa umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu Kofi Annan inasema uhalifu huo wa kikatili na matumizi ya nguvu kupita kiasi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na ni wajibu wa serikali ya Syria wa kusitisha matumizi ya silaha nzito katika maeneo ya raia na pia ghasia za aina yoyote ile.

Jenerali Robert Mood mkuu wa UNSMIS ametoa taarifa isemayo kwamba waangalizi wa Umoja wa Mataifa walienda kwenye kijiji cha Houla ambako walihesabu maiti 32 za watoto wa chini ya miaka 10 na maiti zaidi ya 60 za watu wazima.

Mazingira yaliyosababisha uhalifu na ukatili huo bado hayajafahamika lakini taarifa ya Mood imesema lazima wahusika wawajibishwe. Viongozi wote watatatu wanaitaka serikali ya Syria kusitisha mara moja matumizi ya silaha nzito katika maeneo ya raia na pande zote husika kukomesha mifumo yote ya ghasia.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu zaidi ya 9000 wengi wakiwa raia wameuwaa nchi Syria na maelfu kuwa wakimbizi wa ndani na nje tangu kuzuka maandamano na machafuko ya kumpinga Rais Bashar al-Assad miezi 14 iliyopita.