Somalia Yapiga Marufuku Matumizi ya Bomu za Kutegwa Ardhini licha ya Migogoro

23 Mei 2012

Umoja wa Mataifa umethibitisha leo kuwa Somalia imekuwa nchi ya 160 kuingia katika nchi zilizosaini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya bomu za kutegwa ardhini.

Tangazo hilo limetolewa kwenye mkutano wa wajumbe kutoka zaidi ya mataifa 95 mjini Geneva katika kongamano la kimataifa kujadili hatua zilizochukuliwa kupiga marufuku matumizi ya mabomu ya kuzikwa ardhini.

“Kwa kujiunga kwenye Mkataba wa Kupiga Marufuku mabomu ya ardhini, Somalia imetambua kuwa athari za kibinadamu zinashinda kwa umbali faida zake za kijeshi. Somalia imechukua hatua hii, licha ya kwamba bado kuna mgogoro wa vita ambao unaikumba nchi hiyo, na hivyo inafaa kuigwa na nchi nyigine ambazo zina migogoro ya vita, na zinazosema haziwezi kujiunga kwenye mkataba huo kwa sababu za kiusalama,” amesema Mkurugenzi wa Kampeni ya Kimataifa dhidi ya Mabomu ya kuzikwa ardhini, Kasia Derlicka.

Mabomu ya aina hii ambayo huyaathiri vibaya maisha ya mamia ya watu nchini Somalia, yametumiwa katika miaka mingi ya mizozo, ingawa nchi ya Somalia yenyewe haizalishi mabomu haya. Utafiti ulofanywa mwaka 2008 ulionyesha kuwa takriban jamii 200 katika sehemu 300 tofauti za nchi zinaishi katika hatari ya athari na uangamizaji wa mabomu haya.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter