Makundi ya Kijeshi Somalia yahimizwe yapunguze Athari za vita kwa Raia

23 Mei 2012

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, Mark Bowden, amesema ni lazima lifanywe lolote lile kupunguza athari za mapigano kwa raia, kufuatia kuingia kwa vikosi vya Muungano wa Afrika Somalia, AMISOM na vile vya serikali ya Somalia. Katika taarifa ilotolewa leo, Bwana Bowden pia amesema, makundi yanayozozana ni lazima yaruhusu msaada wa kibinadamu kuwafikia raia wa kawaida.

Ameongeza kuwa ingawa hakuna habari zozote kwa hivi sasa kuhusu raia kukimbia katika eneo hilo la Afgooye, bado ana hofu kuwa hali ikizorota au operesheni hiyo ikichukuwa muda mrefu kukamilishwa, huenda ikachangia watu kutoroka makwao, na hivyo kuziongezea zaidi mzigo jamii zinazowaweka wakimbizi mjini Mogadishu, au kuwafanya watu waende mbali zaidi na maeneo wanakoweza kupata msaada. Hata hivyo, ameongeza kuwa wahudumu wa msaada wa kibinadamu wanafanya maandalizi ya kuhakikisha kuwa msaada unawafikia wale watakaoathiriwa na shughuli za kijeshi katika eneo hilo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter