Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakutana na wakimbizi wa Ivory Coast

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakutana na wakimbizi wa Ivory Coast

Ujumbe wa mabalozi 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao unaongozwa na Balozi wa Marekani Susan Rice na Balozi Mohammed Loulichki wa Morocco, leo umekuwa kwenye mji wa Zwedru kwenye jimbo la Grand Gedeh kukutana na wakimbizi wa Ivory Coast kwenye kambi ya wakimbizi inayopatikana eneo la majengo ya ilokuwa kampuni ya kutengeneza mbao ya Primier, au PTP. Kambi hiyo ndiyo kubwa zaidi katika kambi zote sita za wakimbizi zilizowekwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, pamoja na Tume ya Wakimbizi, Uhamisho na Kutoa Makazi ya Liberia. Kambi ya PTP ina idadi ya zaidi ya wakimbizi 7,200.

Wakati wakiwa kwenye kambi hiyo, wajumbe hao wa Umoja wa Mataifa wamewasikiliza viongozi mbalimbali wa wakimbizi hao wa Ivory Coast, wake kwa waume, wanaowakilisha kambi zote sita zilizomo nchini humo.

Balozi wa Morocco, Mohammed Loulichki ambaye amewahutubia wakimbizi hao kwa niaba ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa, amesema kuwa wamefika hapo kuwaona, na kuwaletea ujumbe wa matumaini kwamba, hivi karibuni, wataziona tena jamii zao katika amani, usalama na utu. Ameusifu pia ukarimu uloonyeshwa na serikali na watu wa Liberia ambao wamewakaribisha majirani wao waliomo katika hali ya unyonge.

Takriban watu 200, 000 walikimbilia Liberia wakitafuta usalama kufuatia uchaguzi ulozozaniwa nchini mwao, Ivory Coast, mwaka 2010. Zaidi ya nusu ya wote waliokimbilia Liberia wamesharejea makwao kufikia sasa kwa juhudi zao wenyewe au wakisaidiwa na UNHCR.