Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani Kushambuliwa kwa rais wa mpito wa Mali

Ban alaani Kushambuliwa kwa rais wa mpito wa Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelaani vikali kushambuliwa na kupigwa kwa rais wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore, kulikomuacha kiongozi huyo wa mpito na majereha kichwani.

Katika taarifa iloyotolewa na msemaji wake, Katibu  Mkuu ametoa wito kwa taasisi za kijeshi na usalama kutimiza wajibu wao wa kimsingi wa kulinda viongozi halali wa mpito na kuhakikisha kuwa wale walotekeleza shambulizi dhidi ya rais wanaadhibiwa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Rais Traore alipigwa jana na waandamanaji ambao waliiteka nyara ikulu ya rais kwa masaa kadhaa wakati wa maandamano yao katika mji mkuu, Bamako. Maandamano hayo yanasemekana kuongozwa na wanasiasa wenyeji ambao wanataka viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Machi warejee mamlakani- ambayo yalilaaniwa na Katibu Mkuu, pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ban ametoa wito kwa wahusika wote nchini Mali kujitenga na vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuchangia kuzorota tena amani na utulivu nchini humo. Wapatanishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi mwa Africa, ECOWAS, walikutana na Baraza la Usalama nchini Ivory Coast tarehe 19 Mei kulizungumzia swala la Mali